WEZI WAIBA NG'OMBE KATIKA MAONYESHO YA WAKULIMA NA WAFUGAJI MOROGORO


Ng'ombe wa Halmashauri ya Temeke jijini ya Jiji la Dar es Salaam, aliyeibwa na wezi usiku wa kuamkia Jumanne wiki hii na kupatikana alfajiri ya jana katika mnada na machinjio ya Nanenane mjini morogoro baada ya kutelekezwa alikopelekwa kuchinjwa, Ng’ombe huyo alikua katika maonyesho ya Walikuma na Wafugaji, Kanda ya Mashariki Uwanja wa Mwl Julius Nyerere Nane Nane yanayoendelea, alipatikana baada ya msako mkali wa Jeshi la Polisi kwa wafanyabiashara wa nyama. Picha na Juma Mtanda

By Lilian Lucas, Morogoro
Watu 49 wana wanashikiliwa na jeshi la polisi mkoani Morogoro kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo ya wizi wa ng’ombe jike aliyeibwa katika Maonyesho ya Wakulima Nanenane kwenye banda la Wilaya ya Temeke pamoja na mtambo wa kutengeneza silaha za kienyeji yakiwepo magobole.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei (pichani)akizungumza na waandishi wa habari jana alisema matukio hayo yalitokea Agosti Mosi na 2 mwaka huu katika maeneo tofauti kwenye wilaya za Mvomero, Kilombero na Manispaa ya Morogoro.

Alisema katika tukio la kwanza watu 43 wa Manispaa ya Morogoro walikamatwa kwenye msako maalumu baada ya kupata taarifa ya kuibiwa kwa ng’ombe jike mwenye madoa meupe na meusi ambaye thamani yake ni Sh3 milioni mali ya Halmashauri ya Wilaya ya Temeke jijini Dar es salaam.

Kamanda Matei alisema ng’ombe huyo aliyekuwa katika banda hilo kwa ajili ya maonyesho ya wakulima na wafugaji nanenane mwaka huu mkoani hapa aliibwa hivyo kulazimu askari wa jeshi la polisi kuanza msako.

Alisema watuhumiwa hao walikamatwa akiwepo mlinzi wa banda hilo, George Lightone (34) mkazi wa Msamvu pamoja na wengine wanaojihusisha na uuzaji wa nyama za wizi katika Manispaa ya Morogoro.

Aidha, alisema kutokana na jitihada zilizofanywa na jeshi hilo, Agosti 4 mwaka huu majira ya Alfajiri eneo la mnada wa mifugo huko Nanenane ng’ombe huyo alipatikana akiwa kafungwa kamba katika nguzo za umeme na kwamba uchunguzi zaidi unaendelea.

Katika tukio jingine katika Kijiji cha Mpanga, Tarafa ya Mlimba wilayani Kilombero askari wakiwa doria walifanikiwa kumkamata na kumpekua Modestus Blastembo maarufu kama Mahanga(80) mkazi wa Kijiji cha Mapanga na kumkuta akiwa na mtambo mmoja wa kutengeneza silaha za kienyeji.

Mtuhumiwa huyo pia alikutwa na magobole manne yaliyotengenezwa kienyeji ndani ya nyumba yake anayoishi na anaendelea kuhojiwa.

Aidha, Kamanda Matei alisema tukio jingine lilitokea katika Kijiji cha Ngalimila Mlimba wilayani Kilombero ambako askari wakiwa doria waliwakamata Antony Athanans (37) na George Bagome (80) wakiwa na silaha moja aina ya gobole lililotengenezwa kienyeji, goroli tisa na baruti moja waliyoihifadhi ndani ya nyumba wanayoishi.

Alisema uchunguzi wa awali unaonyesha watuhumiwa hao hujihusisha na vitendo vya ujangili na wanaendelea kuhojiwa na jeshi la polisi
Share on Facebook