CHAMA CHA WALIMU MVOMERO CHAWAKANYA WALIMU KWA KUWAEPUKA WALAGHAI


CHAMA cha Walimu wilaya ya Mvomero (CWT), kimewatahadharisha walimu kote nchini kuwapuuza na kuwakwepa baadhi ya watu wenye uchu wa madaraka na tamaa ya pesa ambao wanajipitisha kwa walimu wakiwalaghai kuwa waachane na chama chao na badala yake wajiunge na vyama vingine ambavyo vipo kwa ajili ya kutetea maslahi ya walimu.

Akizungumza na MTANDA BLOG mjini hapa, Katibu wa CWT wilaya ya Mvomero, Herry Kavalambi alisema kuwa CWT kinatoa tahadharisha kwa walimu kuwapuuza na kuwakwepa baadhi ya watu wenye uchu wa madaraka na tamaa ya pesa ambao wanajipitisha kwa walimu wakiwalaghai ili kuachana na chama chao.

Kavalambi alisema alitoa ushauri huo kwa walimu baada ya kumalizika kwa mkutano mkuu wa tathmini ya utekelezaji wa majukumu ya chama hicho kwa kipindi cha miaka miwili iliyopita na mpango kazi wake kuelekea mwaka 2020 uliofanyika mwishoni mwa wiki, mkoani hapa.

“Nawasihi walimu tuendelee kushikamana, tutimize wajibu wetu na tukiamini chama chetu,..tuachane na propaganda za vyama vingine vya walimu vilivyosheheni viongozi wenye tamaa ya pesa na uchu wa madaraka...kuendelea kuyumbishwa au kushawishiwa kwa namna yoyote kujiunga na vyama vingine ni kuendelea kujikwamisha sisi wenyewe,” alisema Kavalambi.

Alisema kuwa CWT wilaya ya Mvomero pamoja na mambo mengine imepata mafanikio makubwa nchini ikiwemo kuwaunganisha walimu pamoja tendo lililopelekea ongezeko kubwa la walimu kuzidi kujisajili ndani ya chama hicho hadi kufikia wastani wa asilimia 97 hadi sasa.

Kavalambi alisema kwa umoja wao wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutatua kero mbalimbali za walimu na hasa zile zilizohusisha walimu kusimamishwa kazi bila sababu za msingi, huduma za kisheria, walimu kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya mishahara na utetezi wa wastaafu wanaodai stahili mbalimbali kwa waajiri wao.

“Kwa upande wa walimu walioondolewa kwenye payroll (orodha ya malipo ya mishahara) cwt imekuwa ikiwasaidia posho kidogo za kujikimu na wakati mwingine kusafiri nao hadi kwa waajiri, tumekuwa tukitoa mafunzo ya kisheria, msaada nyakati za majanga, ushauri na unasihi yote haya ni katika kuhakikisha haki na maslahi ya walimu vinazingatiwa”, alisema Kavalambi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa chama hicho, wilaya ya Mvomero, Jumanne Nyakirang’ani, alisema pamoja na mafanikio yaliyopo bado kuna changamoto sugu kwa baadhi ya waajiri kutolipa kwa wakati stahili za walimu hususan likizo, uhamisho na kustaafu.

“Shabaha ya mpango wetu na vipaumbele ni kuhakikisha mwanachama anapata huduma bora eneo lake la kazi ikiwemo uwepo wa maslahi bora na uboreshaji wa miundombinu mbalimbali kwa tija na ustawi, ‘walimu ni kioo’,” alisema Nyakirang’ani.
Share on Facebook